1:1 Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu.
1:2 Hapo kale, Mungu aliwaahidia watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu.
1:3 Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye mintarafu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi;
1:4 mintarafu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka wafu.
1:5 Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii.
1:6 Ninyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo.
1:7 Basi, ninawaandikia ninyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
1:8 Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote.
1:9 Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni
1:10 daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa.
1:11 Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha.
1:12 Ndiyo kusema, tutaimarishana: imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha ninyi.
1:13 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine.
1:14 Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu.
1:15 Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu ninyi mlioko huko Roma.
1:16 Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia.
1:17 Kwa maana Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: "Mwadilifu kwa imani ataishi."
1:18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane.
1:19 Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhirisha.
1:20 Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea!
1:21 Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza.
1:22 Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu.
1:23 Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao.
1:24 Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao.
1:25 Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina.
1:26 Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile.
1:27 Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu.
1:28 Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya.
1:29 Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya,
1:30 na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao;
1:31 hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine.
1:32 Wanajua kwamba Sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.
2:1 Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2:2 Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki.
2:3 Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
2:4 Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?
2:5 Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za haki vitadhihirishwa.
2:6 Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
2:7 Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele.
2:8 Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
2:9 Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
2:10 Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
2:11 Maana Mungu hambagui mtu yeyote.
2:12 Wale wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria.
2:13 Mtu hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii Sheria.
2:14 Mathalan: watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria ingawa hawaijui Sheria.
2:15 Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.
2:16 Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
2:17 Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa wa Mungu;
2:18 kwa njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;
2:19 wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani;
2:20 unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli.
2:21 Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba.
2:22 Unasema: "Msizini," na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu.
2:23 Kwa kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria unamdharau Mungu?
2:24 Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!"
2:25 Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa.
2:26 Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa.
2:27 Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa.
2:28 Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili.
2:29 Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya Sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.
3:1 Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani?
3:2 Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake.
3:3 Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu?
3:4 Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kila usemapo, maneno yako ni ya haki; na katika hukumu, wewe hushinda."
3:5 Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu).
3:6 Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu?
3:7 Labda utasema: "Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!"
3:8 Ni sawa na kusema: tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!
3:9 Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora zaidi kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi.
3:10 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu!
3:11 Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu.
3:12 Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.
3:13 Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
3:14 Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
3:15 Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
3:16 popote waendapo husababisha maafa na mateso;
3:17 njia ya amani hawaijui.
3:18 Hawajali kabisa kumcha Mungu."
3:19 Tunajua kwamba Sheria huwahusu walio chini ya Sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu.
3:20 Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuishika Sheria; kazi ya Sheria ni kumwonyesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.
3:21 Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea Sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili.
3:22 Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote.
3:23 Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu.
3:24 Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa.
3:25 Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonyesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu;
3:26 lakini sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonyesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonyesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humkubali kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
3:27 Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza Sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini.
3:28 Maana mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya Sheria.
3:29 Au je, Mungu nu Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa mataifa mengine pia.
3:30 Mungu ni mmoja, naye atawakubali Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao.
3:31 Je, tunaitumia imani kuibatilisha Sheria? Hata kidogo; bali tunaipa Sheria thamani yake kamili.
4:1 Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu?
4:2 Kama Abrahamu alikubaliwa kuwa mwadilifu kutokana na matendo yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu.
4:3 Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu."
4:4 Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake.
4:5 Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, na hivi humkubali kuwa mwadilifu.
4:6 Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake:
4:7 "Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa.
4:8 Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu."
4:9 Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: "Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu."
4:10 Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa.
4:11 Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu.
4:12 Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.
4:13 Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii Sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu.
4:14 Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii Sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.
4:15 Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna Sheria, haiwezekani kuivunja.
4:16 Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: si kwa wale tu wanaoishika Sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.
4:17 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi." Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini--Mungu ambaye huwapa wafu uzima, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa.
4:18 Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Wazao wako watakuwa wengi kama nyota!"
4:19 Alikuwa mzee wa karibu miaka mia moja, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa.
4:20 Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu.
4:21 Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi.
4:22 Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu.
4:23 Inaposemwa, "Alimkubali," haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu.
4:24 Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka wafu.
4:25 Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na Mungu.
5:1 Sasa, kwa vile tumekubaliwa kuwa wadilifu kwa imani, basi, tunayo amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.
5:2 Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu.
5:3 Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi,
5:4 nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini.
5:5 Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha miminia mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
5:6 Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu.
5:7 Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.
5:8 Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
5:9 Kwa kuwa sasa tumekubaliwa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu.
5:10 Maana, tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo.
5:11 Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu.
5:12 Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi.
5:13 Kabla ya Sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria.
5:14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha yule ambaye atakuja baadaye.
5:15 Lakini ipo tofauti: neema ya Mungu si kama dhambi ya Adamu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake.
5:16 Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu, na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe.
5:17 Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kukubaliwa kuwa waadilifu, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.
5:18 Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kimoja kiadilifu kinawapa uhuru na uzima.
5:19 Na kama kwa kutotii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi wakubaliwe kuwa waadilifu.
5:20 Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.
5:21 Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa njia ya uadilifu, na kuleta uzima wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
6:1 Tuseme nini basi? Je, twendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke?
6:2 Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa--tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi?
6:3 Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake.
6:4 Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.
6:5 Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka wafu kama yeye.
6:6 Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi.
6:7 Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka katika nguvu ya dhambi.
6:8 Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye.
6:9 Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena.
6:10 Hivyo, kwa kuwa alikufa--mara moja tu--dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu.
6:11 Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
6:12 Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake.
6:13 Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni ninyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.
6:14 Maana, dhambi haitawatawala ninyi tena, kwani hamko chini ya Sheria, bali chini ya neema.
6:15 Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya Sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!
6:16 Mnajua kwamba mkijitolea ninyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo--au watumwa wa dhambi, na matokeo yake ni kifo, au wa utii, na matokeo yake ni kukubaliwa kuwa waadilifu.
6:17 Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini--namshukuru Mungu--mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.
6:18 Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu.
6:19 (Hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe.) Kama vile wakati fulani mlivyojitolea ninyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu.
6:20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na uadilifu.
6:21 Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo!
6:22 Lakini sasa, mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uzima wa milele.
6:23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uzima wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.
7:1 Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua Sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai.
7:2 Mathalan: mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuw hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke.
7:3 Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi.
7:4 Hali kadhalika ninyi ndugu zangu: ninyi pia mmekufa kuhusu Sheria kwa kuwa ninyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu.
7:5 Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na Sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo.
7:6 Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya Sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya Sheria iliyoandikwa.
7:7 Je, tuseme basi, kwamba Sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila Sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama Sheria isingalikuwa imesema: "Usitamani."
7:8 Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila Sheria dhambi ni kitu kilichokufa.
7:9 Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na Sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka,
7:10 nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo.
7:11 Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua.
7:12 Basi, Sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri.
7:13 Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Iliyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionyesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno.
7:14 Tunajua kwamba Sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi.
7:15 Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachochukia ndicho nikifanyacho.
7:16 Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile Sheria ni nzuri.
7:17 Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi iliyo ndani yangu.
7:18 Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza.
7:19 Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka.
7:20 Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi iliyo ndani yangu.
7:21 Basi, nimegundua kanuni hii: ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua.
7:22 Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu.
7:23 Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu.
7:24 Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka katika mwili huu unaonipeleka kifoni?
7:25 Shukrani kwa Mungu afanyaye hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya dhambi.
8:1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo.
8:2 Maana, sheria ya Roho iletayo uzima kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.
8:3 Mungu ametekeleza jambo lile ambalo Sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu w binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi.
8:4 Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya Sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho.
8:5 Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho.
8:6 Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uzima na amani.
8:7 Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii.
8:8 Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
8:9 Lakini ninyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo.
8:10 Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu itakufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmekubaliwa kuwa waadilifu.
8:11 Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka wafu ataipa uzima miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
8:12 Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu.
8:13 Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi.
8:14 Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu.
8:15 Kwa maana, Roho mliyempokea si Roho mwenye kuwafanya ninyi watumwa na kuwatia tena hofu; sivyo, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya ninyi watoto wa Mungu, na kwa nguvu ya huyo Roho, sisi tunaweza kumwita Mungu, "Aba," yaani "Baba!"
8:16 Naye Roho mwenyewe anajiunga na roho zetu na kuthibitisha kwamba sisi ni watoto wa Mungu.
8:17 Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.
8:18 Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyafananisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu.
8:19 Viumbe vyote vinatazamia kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake.
8:20 Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini,
8:21 maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu.
8:22 Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto.
8:23 Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukitazamia kufanywa watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe.
8:24 Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa; lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona?
8:25 Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu.
8:26 Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka.
8:27 Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu.
8:28 Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kufuatana na kusudi lake.
8:29 Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
8:30 Basi, Mungu aliwaita wale aliokuwa amewateua; na hao aliowaita aliwakubali kuwa waadilifu; na hao aliowakubali kuwa waadilifu aliwashirikisha pia utukufu wake.
8:31 Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga?
8:32 Mungu hakumhurumia hata mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote?
8:33 Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia!
8:34 Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea!
8:35 Ni nani awezaye kututenga na mapendo ya Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kuuawa?
8:36 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha: tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa."
8:37 Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda.
8:38 Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: wala kifo, wala uhai; wala malaika, au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka;
8:39 Wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu kwetu kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.
9:1 Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia.
9:2 Nataka kusema hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu
9:3 kwa ajili ya watu wangu, walio damu moja nami! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi kulaaniwa na kutengwa na Kristo.
9:4 Hao ndio watu wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake.
9:5 Wao ni wajukuu wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao. Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.
9:6 Sisemi kwamba ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu.
9:7 Wala, si wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Wazao wake watatokana na Isaka."
9:8 Nido kusema, wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake.
9:9 Maana ahadi yenyewe ni hii: "Nitakujia wakati maalum, naye Sara atapata mtoto."
9:10 Tena si hayo tu ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu.
9:11 Lakini, ili Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya,
9:12 Rebeka aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu.
9:13 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia."
9:14 Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo!
9:15 Maana alimwambia Mose: "Nitamhurumia mtu yeyote ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka."
9:16 Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au mapenzi ya mtu.
9:17 Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao: "Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina langu litangazwe popote duniani."
9:18 Ni wazi, basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo.
9:19 Labda utaniuliza: "Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?"
9:20 Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: "Kwa nini umenitengeneza namna hii?"
9:21 Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na kingine kwa matumizi ya kawaida.
9:22 Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonyesha ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake, Basi, alikuwa na saburi sana, akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili kuangamizwa.
9:23 Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha kututayarisha kuupokea utukufu wake.
9:24 Maana sisi ndio hao aliowaita, si tu kutoka miongoni mwa Wayahudi bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine.
9:25 Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea: "Wale waliokuwa Si watu wangu nitawaita: Watu wangu! Naye Sikupendi ataitwa: Mpenzi wangu!
9:26 Na pale walipoambiwa: Ninyi si wangu hapo wataitwa: Watoto wa Mungu hai."
9:27 Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaaza sauti: "Hata kama watoto wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaookolewa;
9:28 maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu ya ulimwengu wote."
9:29 Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: "Kama Bwana Mwenye Nguvu asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa kama Sodoma, tungalikwisha kuwa ma Gomora."
9:30 Basi, tuseme nini? Ni hivi: watu wa mataifa ambao hawakutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu, wamekubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani,
9:31 hali watu wa Israeli waliokuwa wakitafuta Sheria iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu, hawakuipata.
9:32 Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa
9:33 kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Tazama! Naweka huko Sioni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa!"
10:1 Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima.
10:2 Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli.
10:3 Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu.
10:4 Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu.
10:5 Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi."
10:6 Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: Nani atapanda mpaka mbinguni? (yaani, kumleta Kristo chini);
10:7 wala usiseme: Nani atashuka mpaka Kuzimu (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)."
10:8 Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri.
10:9 Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka.
10:10 Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa.
10:11 Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika."
10:12 Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao.
10:13 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa."
10:14 Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri?
10:15 Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!"
10:16 Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?"
10:17 Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.
10:18 Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu."
10:19 Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu."
10:20 Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu."
10:21 Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii."
11:1 Basi, nauliza: je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mini binafsi ni Mwisraeli mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini.
11:2 Mungu hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko Matakatifu juu ya Eliya wakati alipomnung'unikia Mungu kuhusu Israeli:
11:3 "Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua?"
11:4 Je, Mungu alimjibu nini? Alimwambia: "Nimejiwekea elfu saba ambao hawakumwabudu Baali."
11:5 Basi, ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu aliwateua kwa sababu ya neema yake.
11:6 Uteuzi wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.
11:7 Sasa, je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa,
11:8 kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao."
11:9 Naye Daudi anasema: "Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na kuadhibiwa.
11:10 Macho yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!"
11:11 Basi, nauliza: je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate kuwaonea wivu.
11:12 Kosa la Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao kwa kiroho umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri zaidi kwamba utimilifu wao utasababisha baraka nyingi zaidi.
11:13 Basi, sasa nawaambieni ninyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu,
11:14 nipate kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee ninyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa baadhi yao.
11:15 Maana ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!
11:16 Ikiwa kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia.
11:17 Naam, baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la mzeituni mwitu likapandikizwa. Ninyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini.
11:18 Basi, msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia, kumbukeni kwamba si ninyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo inayowategemeza ninyi.
11:19 Lakini utasema: "Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake."
11:20 Sawa! Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako. Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari.
11:21 Kwa maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je, unadhani atakuhurumia wewe?
11:22 Kumbuka, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la sivyo, nawe pia utakatwa.
11:23 Nao Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.
11:24 Ninyi watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.
11:25 Ndugu zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana. Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine watakapokuwa wamemfikia Mungu.
11:26 Hapo ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Mkombozi atakuja kutoka Sioni, atauondoa uovu wa Yakobo.
11:27 Hili ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao."
11:28 Kwa sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa adui wa Mungu, lakini kwa faida yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni rafiki wa Mungu kwa sababu ya baba zao.
11:29 Maana Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo.
11:30 Hapo awali ninyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na kuasi kwao.
11:31 Hali kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa ninyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu.
11:32 Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili wapate kuwahurumia wote.
11:33 Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
11:34 "Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake?
11:35 Au, nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kulipwa tena kitu hicho?"
11:36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake. Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina.
12:1 Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
12:2 Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
12:3 Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
12:4 Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
12:5 Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
12:6 Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
12:7 Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
12:8 Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
12:9 Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.
12:10 Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima.
12:11 Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
12:12 Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima.
12:13 Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
12:14 Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani.
12:15 Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia.
12:16 Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana.
12:17 Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
12:18 Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.
12:19 Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana."
12:20 Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake."
12:21 Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.
13:1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu.
13:2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe,
13:3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu;
13:4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu kwao watendao maovu.
13:5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo.
13:6 Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao.
13:7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.
13:8 Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza Sheria.
13:9 Maana, amri hizi: "Usizini; Usiue; Usitamani;" na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."
13:10 Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, kwa mapendo Sheria yote hutimizwa.
13:11 Zaidi ya hayo, ninyi mnajua tumo katika wakati gani: sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu u karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini.
13:12 Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga.
13:13 Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana; tusiwe na ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu.
13:14 Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.
14:1 Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi.
14:2 Watu huhitilafiana: mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani.
14:3 Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali.
14:4 Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha.
14:5 Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake.
14:6 Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu.
14:7 Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe
14:8 maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana.
14:9 Maana Kristo alikufa, akafufuka ili wapate kuwa Bwana wa wazima na wafu.
14:10 Kwa nini, basi wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
14:11 Maana Maandiko yanasema: "Kama niishivyo, asema Bwana kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu."
14:12 Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja yake mbele ya Mungu.
14:13 Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu yetu au kumsababisha aanguke katika dhambi.
14:14 Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi.
14:15 Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na mapendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake!
14:16 Basi, msikubalie kitu mnachokiona kuwa kwenu ni kitu chema kidharauliwe.
14:17 Maana Utawala wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.
14:18 Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu.
14:19 Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana.
14:20 Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi.
14:21 Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke.
14:22 Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake.
14:23 Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.
15:1 Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu.
15:2 Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani.
15:3 Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: "Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi."
15:4 Maana yote yalioandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na Maandiko hayo Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
15:5 Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni ninyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,
15:6 ili ninyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
15:7 Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni.
15:8 Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonyesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia;
15:9 ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa sababu hiyo, nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako."
15:10 Tena Maandiko yasema: "Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake."
15:11 Na tena: "Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni."
15:12 Tena Isaya asema: "Atatokea mtu katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia."
15:13 Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
15:14 Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba ninyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi.
15:15 Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu
15:16 ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, dhabihu iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
15:17 Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu.
15:18 Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo,
15:19 kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo.
15:20 Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
15:21 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Watu wote ambao hawakuambiwa habari zote wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa."
15:22 Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu.
15:23 Lakini maadam sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu,
15:24 natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi.
15:25 Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalem.
15:26 Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoka mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalem.
15:27 Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia.
15:28 Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni ninyi nikiwa safarini kwenda Spania.
15:29 Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.
15:30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa ajili ya upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu.
15:31 Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalem ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko.
15:32 Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi.
15:33 Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!
16:1 Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea.
16:2 Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia.
16:3 Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu.
16:4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine.
16:5 Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao. Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni kwa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo.
16:6 Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
16:7 Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi.
16:8 Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana.
16:9 Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku.
16:10 Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
16:11 Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana.
16:12 Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana.
16:13 Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia.
16:14 Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
16:15 Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olumpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.
16:16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo.
16:17 Ndugu zangu, nawasihi muwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao,
16:18 maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu.
16:19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu na hivyo mmekuwa sababu ya furaha yangu. Nawatakeni muwe na hekima katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya.
16:20 Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
16:21 Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipatro, wananchi wenzangu, wanawasalimu.
16:22 Nami Tertio, ninayeandika barua hii nawasalimuni katika Bwana.
16:23 Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu.
16:24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.
16:25 Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya ujumbe wa Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita.
16:26 Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirisha kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii.
16:27 Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina.