Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 1 Peter

1:1 Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia.

1:2 Mungu Baba aliwateua ninyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele.

1:3 Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Ametujalia tumaini lenye uzima,

1:4 na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza au kuharibika au kufifia.

1:5 Hizo zitakuwa zenu ninyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati.

1:6 Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka.

1:7 Shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu ambayo ni ya thamani zaidi kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima Siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.

1:8 Ninyi mnampenda ingawaje hamjamwona, na mnamwamini ingawa hamumwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka,

1:9 kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu.

1:10 Manabii walipeleleza kwa makini na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo ninyi mngepewa.

1:11 Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata.

1:12 Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo ninyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.

1:13 Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa kwa nia, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika baraka ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana!

1:14 Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga.

1:15 Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu.

1:16 Maandiko yasema: "Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu."

1:17 Mnapomtaja Mungu ninyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu.

1:18 Maana mnajua kwamba ninyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu, si kwa vitu vyenye kuharibika: kwa fedha na dhahabu;

1:19 bali mlikombolewa kwa damu tukufu ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwana kondoo asiye na dosari wala doa.

1:20 Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.

1:21 Kwa njia yake, ninyi mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu.

1:22 Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, ninyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote.

1:23 Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, ninyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele.

1:24 Kama Maandiko yasemavyo: "Kila binadamu ni kama nyasi, na utukufu wake wote ni kama maua ya porini. Nyasi hunyauka na maua huanguka.

1:25 Lakini neno la Bwana hudumu milele." Neno hilo ni hiyo Habari Njema iliyohubiriwa kwenu.

2:1 Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena.

2:2 Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa.

2:3 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua kwamba Bwana ni mwema."

2:4 Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa.

2:5 Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

2:6 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."

2:7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi."

2:8 Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.

2:9 Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.

2:10 Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.

2:11 Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.

2:12 Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake.

2:13 Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,

2:14 utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.

2:15 Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.

2:16 Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu.

2:17 Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme.

2:18 Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza.

2:19 Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili.

2:20 Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo.

2:21 Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake.

2:22 Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.

2:23 Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.

2:24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.

2:25 Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.

3:1 Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno,

3:2 kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu.

3:3 Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi.

3:4 Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu.

3:5 Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao.

3:6 Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Ninyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote.

3:7 Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uzima anayowapeni Mungu. Hapo ndipo sala zenu hazitakataliwa.

3:8 Mwisho nasema hivi: mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kidugu, kuwa wapole na wanyenyekevu ninyi kwa ninyi.

3:9 Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana ninyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka.

3:10 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, anapaswa kuacha kusema mabaya na kuacha kusema uongo.

3:11 Na ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia.

3:12 Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu."

3:13 Ni nani atakayeweza kuwadhuru ninyi kama mkizingatia kutenda mema?

3:14 Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi.

3:15 Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu,

3:16 lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu.

3:17 Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu.

3:18 Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke ninyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho;

3:19 na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni.

3:20 Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa majini,

3:21 ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa ninyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo,

3:22 ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.

4:1 Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi.

4:2 Tangu sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu.

4:3 Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu.

4:4 Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni.

4:5 Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu wazima na wafu!

4:6 Kwa sababu hiyo, hao waliokufa ambao walikuwa wamehukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama anavyohukumiwa kila mmoja, walihubiriwa Habari Njema kusudi katika maisha yao ya kiroho waishi kama aishivyo Mungu.

4:7 Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na nidhamu, ili mweze kusali.

4:8 Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi.

4:9 Muwe na ukarimu ninyi kwa ninyi bila kunung'unika.

4:10 Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu.

4:11 Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.

4:12 Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida.

4:13 Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa.

4:14 Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu.

4:15 Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni muuaji, mwizi, mhalifu au mwovu.

4:16 Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo.

4:17 Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu?

4:18 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?"

4:19 Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.

5:1 wazee! Mimi niliye mzee ninalo ombi moja kwenu wazee wenzangu. Mimi mwenyewe nilishuhudia kwa macho yangu mateso ya Kristo na natumaini kuushiriki ule utukufu utakaofunuliwa. Mimi nawaombeni

5:2 mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote.

5:3 Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi.

5:4 Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, ninyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia.

5:5 Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Ninyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu."

5:6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao.

5:7 Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni.

5:8 Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo.

5:9 Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo.

5:10 Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni muushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara.

5:11 Kwake uwe uwezo milele! Amina.

5:12 Nimewaandikieni barua hii fupi kwa msaada wa Silwano, ndugu ambaye namjua na kumwamini. Nataka kuwapeni moyo na kushuhudia kwamba jambo hili ni neema ya Mungu kweli. Kaeni imara katika neema hiyo.

5:13 Jumuiya ya wenzenu walioteuliwa na Mungu hapa Babuloni wanawasalimuni. Vilevile mwanangu Marko anawasalimuni.

5:14 Salimianeni kwa ishara ya upendo wa Kikristo. Nawatakieni amani ninyi mlio wake Kristo.


Next: 2 Peter