Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 2 Peter

1:1 Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.

1:2 Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

1:3 Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.

1:4 Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.

1:5 Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu,

1:6 kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu,

1:7 udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.

1:8 Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

1:9 Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani.

1:10 Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe.

1:11 Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

1:12 Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea.

1:13 Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.

1:14 Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.

1:15 Basi, nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya kufariki kwangu.

1:16 Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe.

1:17 Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye."

1:18 Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu.

1:19 Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong'ara mioyoni mwenu.

1:20 Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu.

1:21 Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

2:1 Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo walimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe.

2:2 Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, kwa sababu yao, wengine wataipuuza Njia ya ukweli.

2:3 Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yu tayari, na Mwangamizi wao yu macho!

2:4 Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea Siku ile ya Hukumu.

2:5 Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba.

2:6 Mungu aliadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu.

2:7 Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi.

2:8 Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu.

2:9 Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi Siku ile ya hukumu,

2:10 hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni washupavu na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu.

2:11 Lakini malaika, ambao wana uwezo na nguvu zaidi kuliko hao walimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana.

2:12 Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili, ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe,

2:13 na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, bali wakifurahia njia zao za udanganyifu.

2:14 Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu!

2:15 Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori, ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu,

2:16 akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii.

2:17 Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu.

2:18 Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu.

2:19 Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu--maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala.

2:20 Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali.

2:21 Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kujua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea.

2:22 Ipo mithali isemayo: "Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe," na nyingine isemayo: "Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!" Ndivyo ilivyo kwao sasa.

3:1 Wapenzi wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya.

3:2 Napenda mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa na mitume wenu.

3:3 Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki ninyi

3:4 na kusema: "Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!"

3:5 Watu hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na nchi zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji;

3:6 na kwa maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa.

3:7 Lakini mbingu na nchi za sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya Siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa.

3:8 Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja.

3:9 Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu.

3:10 Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake.

3:11 Maadamu kila kitu kitaharibiwa namna hiyo, je, ninyi mnapaswa kuwa watu wa namna gani? Mnapaswa kuishi kitakatifu na kumcha Mungu,

3:12 mkiingojea Siku ile ya Mungu na kuifanya ije upesi--Siku ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na vitu vyake vya asili vitayeyushwa kwa joto.

3:13 Lakini sisi, kufuatana na ahadi yake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu.

3:14 Kwa hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnangojea Siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye.

3:15 Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa, kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na Mungu.

3:16 Hayo ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga, wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe.

3:17 Lakini ninyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara.

3:18 Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.


Next: 1 John